Friday, October 29, 2010

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI (MMBA) LOLIONDO;

Mpango wa matumizi bora ya ardhi (Land Use Plan) ni mfumo madhubuti unaohusisha majadiliano kati ya wadau wote ili kulenga makubaliano, and maamuzi juu ya mpango endelevu wa ardhi katika maeneo ya vijijini lakini pia kuanzisha na kusimamia utekelezaji wake.
Mpango wa matumizi bora ya ardhi upo katika jamii yoyote hata pale ambapo neno hili halitumiki, mpango huu umeanza katika nchi zinazoendelea miaka ya 1980s (Amler et al 1999)[1].
Mpango huu hufuata kanuni zake ili uweze kutimiza lengo husika, kanuni hizi hazitofautiana sana kutoka Mpango wa matumizi bora ya ardhi hutoa fursa ya kuvuna mpango endelevu wa matumizi ya ardhi inayokubalika kulingana na matakwa ya kijamii na kimazingira husika na inaaminiwa na kupokelewa na jamii wakati wanafanya uchanganuo wa kijamii na kiuchumi (social and economic sense).
sehemu moja hadi nyingine,japo wakati mwingine kunakuwa na tofauti kulingana na aina ya mradi na malengo ya mradi.
Baadhi ya kanuni hizo ni (principles of land use plan) (ibid);
ü MMBA chanzo chake kikuu ni hali ya kawaida ya sehemu kwa kuangalia yote mbinu zitakazo tumika na lengo kuu (methods and content).
ü MMBA inaangalia zaidi mtazamo wa mila au desturi na hujengwa ndani ya uwelewa wa mazingira ya jadi.
ü MMBA huzingatia zaidi mbinu za jadi za utatuzi wa migogoro na matatizo mengine.
ü MMBA pia huangalia suala la Maendeleo vijijini kuwa ni mfumo unaoanza chini-juu (bottom – up) ambao hutoa fursa ya uwajibikaji.
ü MMBA ni mdahalo unaojenga na kuleta mazungumzo na makubaliano juu ya kipi kifanyike baada ya makubaliano na wadau wa Maendeleo.
ü MMBA ni mfumo unaopelekea kujengeka kwa uwezo wa washiriki kuweza kuweka mipango na kufanya utekelezaji.
ü MMBA unahitaji uwazi, na hivyo uhuru wa kupata taarifa.
ü Ushiriki wa wadau wote na pia kufuata jinsia ni masuala muhimu katika MMBA.
ü MMBA ni mfumo unaoruhusu muingiliano wa fani mbalimbali (interdisciplinary).
ü MMBA ni mfumo unaobadilika na kuruhusu mabadiliko (flexible and open).
ü MMBA ni utekelezaji.

MMBA nchini Tanzania imeanzishwa mnamo miaka ya 1990s na ikaanzishwa Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya ardhi (NLUPC) lengo lake kuu ni kuweka pamoja(harmonise) na kuunganisha (Co-ordinate) sera, sheria za matumizi ya ardhi pamoja na kukuza ulindaji na uendelezaji wa ardhi nzuri kwa lengo la kuhakikisha utumiaji endelevu wa ardhi ili kuleta uzalishaji wenye tija na kurahisisha maendeleo kwa uzalishaji wa baadaye. Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi inafanyakazi nchi nzima ikishirikiana na wadau wote ardhi kwanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini(www.nlupc.or.tz[2] ).
Tarafa ya Loliondo, ni sehemu ya Mkoa wa Arusha, Wilayani Ngorongoro kaskazini mwa Tanzania, ipo 2°15" S na 35°30"E, linakadiriwa kuwa na ukubwa eneo la 289,800 ha. Mgawanyo wa matumizi ya ardhi katika tarafa ya Loliondo ni kama ifuatavyo kwenye jedwali;

Land Use Category
Area (Ha)
Percentage

Agriculture
8078.0
2.8

Forest
8850.0
3.1

Range Land/Game Reserve Area
236,908.0
81.7

Settlement/Service Infrastructure
35,963.0
12.4
Chanzo: Agriculture department – Loliondo division 1990/91 in Mtorani. V.L (1997:4)
Tume ya Taifa ya Tanzania ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC) ya mwaka 1994 wanabainisha kuwa kuna aina nne ya matumizi ya ardhi katika tarafa ya Loliondo ambazo ni kilimo cha kujikimu, ufugaji usio na mipango (unplanned livestocking), ardhi ya hifadhi na makazi (Loliondo Land Use Plan, 1994[3]).
Pia Mtorani. V.L (1997:3) anaeleza kuwa mipango inawekwa au kupangwa na Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi ili kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi ya loliondo lengo kuu ni kutatua na kuboresha hali ya chakula na kupunguza ukame ulioripotiwa kabla ya miaka ya 1990s.
Eneo la Tarafa ya Loliondo kwa ujumla limevuta hisia za wengi popote dunia mnamo mwishoni mwa mwaka 2009 pale palipozuka mgogoro kati ya Kampuni ya uwindaji ya OBC ikishirikiana na vikosi vya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilipo vamia na kuchoma moto maboma ya jamii ya Kimasai wanaoishi karibu na eneo la Kitalu cha uwindaji. Lakini pia zoezi zima la kuchoma maboma na kuhamisha wamasai katika eneo hilo limegubikwa na utata wa ukiukwaji wa haki za binadamu kama ubakaji, uchomaji wa maboma, watu kupigwa na watoto kuripotiwa kupotea kabisa. Baada ya suala zima kuwa katika hali isiyo ya kawaida, serikali ya Jamhuri kupitia Bunge ilituma kamati ya Maliasili na Mazingira chini ya mwenyekiti wake Job Ndugai Mbunge wa Kongwa (CCM) kuchukuwa maoni ya wananchi na wadau wengine juu ya suala zima, lakini mpaka sasa ripoti ya Ndugai bado haijulikani ilipo na maoni na mapendekezo ya wanaharakati wa haki za binadamu yamewekwa wapi.
Pia, mwishoni mwa mwezi Februari 26th 2010, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh.John Chiligati na Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na matumizi bora ya Ardhi, walitembelea Tarafa ya Loliondo na kusema kuwa serikali imepata mwarobaini wa ufumbuzi wa migogoro ya ardhi wilayani Ngorongoro, ambapo sh milioni 156.7 zimetengwa kwa ajili ya kupima vijiji na kutoa hati miliki kwa vijiji na utaratibu huo kuanza machi 2010 hadi juni 2010 (Nipashe 25/02/2010 page 8[4]).
Sambamba na hayo, kabla kidonda hakijapona tarehe 31st Machi 2010 na 7th Aprili 2010 wanawake wa wilaya ya Ngorongoro hasa tarafa ya Loliondo zaidi ya akina mama 200 walikwenda katika ofisi ya chama tawala (CCM) yaliyopo Loliondo na kurudisha kadi zao kwa madai kuwa serikali chini ya CCM imeshindwa kuwaboreshea maisha na zaidi serikali inawaonea kwani 2009 walikuwa na mgogoro na OBC sasa tume imefika kugawa maeneo yao bila wao kujulishwa na maeneo yanatengwa kwajili ya wanyamapori bila wao kupata pakulishia mifugo yao. Maandamano hayo ya akina mama imepelekea wanaharakati wa haki za binadamu watatu kuwekwa rumande kwajili ya kuwa ndio waendesha maandamano ya wanawake hao.
Lakini pia Mkuu wa Wilaya hiyo Wawa Lali alisikika kwenye TV ya ITV akisema kuwa wanawake hao hawana madai ya msingi kwani tayari wilaya imeshapanga matumizi bora ya ardhi na suala kubwa ni kuwa mfumo dume wa mila ya Kimasai ya wanawake kutokuwa na sauti katika maamuzi.
Kutokana na hayo yote nimesukumwa kuandika kuhusu ushirikishwaji katika kupanga matumizi bora ya ardhi nchini Tanzania na sana sana Tarafa ya Loliondo.
Katika kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi popote pale duniani na Tanzania kwa ujumla kuna mambo au kanuni zinazotakiwa zifuatwe ili kutimiza lengo kuu la MMBA. Kanuni zipo nyingi ila nitazungumzia baadhi tu kwa kuangalia yanayotokea Loliondo Ngorongoro.
Kwanza, inaangalia zaidi mtazamo wa mila au desturi na hujengwa ndani ya uwelewa wa mazingira ya jadi. Hii ikiwa na maana kuwa MMBA inatokana na mtazamo wa mila na desturi ya watu waishio katika eneo husika (LUP considers cultural view points and builds up on local environmental knowledge).
Kwa Loliondo wenyeji ni wamasai wanachukuwa asilimia 90 ya wakazi wa tarafa ya Loliondo na wamekuwepo hapo kwa maisha yao yote na hivyo wana mbinu za jadi za matumizi bora ya ardhi. Swali linakuja je ni mtazamo wa desturi au mila gani inatumiwa na wafuasi wa MMBA huko Loliondo?
Pili, MMBA huzingatia zaidi mbinu za jadi za utatuzi wa migogoro na matatizo mengine. Maana yake ni kuwa ili MMBA ifanikiwe lazima izingatie mbinu na taratibu zinazotumiwa na wenyeji kutatua matatizo yao.
Kwa eneo la Loliondo linalokaliwa kwa sehemu kubwa na wamasai pia wanataratibu zao za utatuzi wa migogoro na hivyo MMBA ikishirikiana na wenyeji basi migogoro itaisha. Mh. John Chiligati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipotembelea tarafa ya Loliondo mwshinoni mwa Februari, 2010 alisema kuwa sasa serikali imepata mwarobaini wa matatizo ya Loliondo kwa kutekeleza MMBA lakini kabla hata mwezi haujaisha ambao ni Machi aliosema Waziri kuwa ndio ardhi itaanza kupimwa tayari maandamano yameanza na madai ni kuwa ardhi inapimwa bila kushirikisha wananchi.
Hapa tena swali linakuja ni mbinu zipi MMBA inatumia katika kufikisha ujumbe wao kwa wananchi? au ni nani yupo nyuma ya MMBA maana kama MMBA ni chombo kinachojitegemea (huru)basi bila shaka wenyeji wangeulizwa mbinu zao za utatuzi wa migogoro na ambazo pia zingeweza kusaidia kutatua mgogoro usioisha loliondo.
Tatu, MMBA pia huangalia suala la Maendeleo vijijini kuwa ni mfumo unaoanza chini-juu (bottom – up) ambao hutoa fursa ya uwajibikaji (self help and self responsibility). Hapa tena tunaona kuwa lengo kuu la MMBA ni kuanzia ngazi ya chini kwenda juu, kwa maana hiyo wenye neno zaidi ni wanyeji kwani ‘Maendeleo’ ni kwajili ya wao hivyo MMBA huangalia vipaumbele vya Maendeleo vya umma wa eneo husika. Kwa mtazamo wa kina Maendeleo Loliondo ni kwa ajili ya nani wenyeji waishio hapo, ‘serikali’ au makampuni ya Wawekezaji yenye uwezo wa kuchangia ‘pato’ la Taifa? Na nini hasa maana ya Maendeleo?
Nne, MMBA ni mdahalo unaojenga na kuleta mazungumzo na makubaliano juu ya kipi kifanyike baada ya makubaliano na wadau wa Maendeleo (LUP is a dialogue, creating a prerequisites for successful negotiation and co-operation among stakeholders). Kanuni hii ya MMBA inatoa fursa kwa wadau wote wa ardhi uhusika kuwa na mazungumzo na hatimaye kufikia hitimisho ambalo linatokana na makubaliano yan wote. Kwa tarafa ya Loliondo wadau wa Maendeleo ni wengi zipo asasi za kiraia,taasisi za serikali, kampuni mbalimbali za Wawekezaji na pia wenyeji ambao ndio wengi.
Swali lingine hapa linakuja kuwa mdahalo uliendeshwa wapi, lini, kati ya nani na nani na wapi makubaliano ya pamoja juu ya matumizi ya ardhi ya Loliondo?.
Tano, MMBA ni mfumo unaopelekea kujengeka kwa uwezo wa washiriki kuweza kuweka mipango na kufanya utekelezaji (LUP is a process leading to an improvement in the capacity of the participants to plan and take actions).
Kwa yanayo toke Loliondo sasa ndivyo sivyo kwani washiriki kisheria hawashirikishwi na kama wanashirikishwa ni sehemu ndogo sana, na hakuna wanachosaidiwa ili nao waweze kung’amua japo angalau kidogo kuhusu utaalamu huo.
Sita, MMBA unahitaji uwazi, na hivyo uhuru wa kupata taarifa (LUP requires transparency).
Sambamba na hayo yote hapo juu, MMBA inazingatia pia kanuni ya uwazi na uhuru wa upatikanaji wa taarifa. Taarifa ya MMBA katika tarafa ya Loliondo imejulikana rasmi na umma mwezi Februari 2010 pale Waziri alipotamka na kuandikwa katika vyombo vya habari kuwa sasa MMBA Loliondo, lakini ukiangalia katika marejeo (literatures) mbalimbali utagundua kuwa taarifa ilikuwepo na Tume ya Taifa ya Mipango Bora ya Matumizi Bora ya Ardhi inayo ardhi ya Loliondo na ipo mpaka katika kumbukumbu za kisayansi ya Geo toka miaka ya 1994 (Loliondo Area a typical Geo Information case 1994-2008 (angalia Mtorani, V.L, 1997:3).
Kwa mtazamo tu wa kawaida na wa mtu yeyote wa ngazi yoyote, utagunduwa kuwa uwazi upo wapi katika MMBA, kama taarifa zipo katika maandishi ni lini wahusika wamepanga matumizi hayo na ni wapi walikaa wakati wanapima ardhi ya wenyeji? Mbali na hilo wananchi wa eneo husika wana uhuru wa kupata taarifa juu ya ardhi yao lakini nani atatoa taarifa kama mambo ndo hayo yaani ardhi ilishapangiwa matumizi miaka ishirini iliyopita bila wenyeji kujua lakini inapofika utekelezaji ndio wananchi wanalaumiwa kwa kisingizio kuwa hawataki Maendeleo au kama anavyosema DC wa Ngorongoro Wawa Lali ni mila ‘potofu’.
Saba, Ushiriki wa wadau wote na pia kufuata jinsia ni masuala muhimu katika MMBA (the differentiation of stakeholders and the gender approach are principles in LUP). Ili MMBA iwe endelevu lazima izingatie aina mbalimbali za washiriki kwa jicho la jinsia. Maana kuu hapa ni kuwa utumiaji na utunzaji wa rasilimali ardhi unahusisha jinsia na sio jinsi hivyo wanawake wana mchango mkubwa katika matumizi bora ya ardhi na hivyo ushiriki wao ni wa maana sana.
Kwa tarafa ya Loliondo, pamoja na kwamba mipango ya matumizi bora ya ardhi yalikwisha fanywa zamani (miaka ishirini iliyopita) na haijulikani nani haswa ameshirikishwa swala la jinsia halijaacha kutokea. Mwanzoni mwa Aprili 2010, wanawake kutoka Loliondo waliandamana hadi ofisi za CCM huko Loliondo kwa madai kuwa wanyanyaswa na serikali iliyo madarakani ya CCM na hivyo hwapo tayari kuendelea kushuhudia wakinyanyaswa na CCM, madai yao makubwa ni kutoshirikishwa kama wanawake na kama jamii katika maamuzi ya matumizi ya ardhi yao.
Kutokana na baadhi ya Kanuni hizi saba za MMBA nilizo zianisha hapo juu, tunajifunza kuwa maswali mengi yaliyojitokeza ndiyo yanayotawala mgogoro wa Loliondo na bila kuyajibu yote kwa wananchi basi mwarobaini wa matatizo ya Loliondo bado haujapatikana bali wananchi wanakumbushwa tu yaliyowasibu miaka ya 1950s walipopokwanywa ardhi yao yenye rutuba na waingereza na hivyo kuendelea kuonekana wazururaji katika ardhi ya mababu zao.
Naomba nisieleweke kuwa napinga MMBA la hasha, nachokataa hapa ni kutokuwepo kwa ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya msingi hasa ardhi na mbali zaidi watu ambao wameshajeruhiwa na wanauguza majeraha. (Kuna usemi usemao kuwa ‘aliyeumwa na nyoka hata akiguswa na kijiti lazima aruke akidhani ni nyoka’).
Kutokana na matukio yanayotokea Loliondo, mengi yanatokana na sheria zisizorafiki na wafugaji wa eneo lile na maeneo mengine yanayokaliwa na wazalishaji wadogowadogo na pia wimbi la Wawekezaji wanaotafuta makazi katika eneo la Loliondo kwa shughuli zao za kibiashara bila hata kushirikisha wenyeji wa pale.
Nini kifanyike/ Mapendekezo
Eneo la Loliondo pamoja na kuwa linakaliwa kwa sehemu kubwa na jamii ya wafugaji ni eneo lilo katika hifadhi ya wanyapori, kitalu cha uwindaji cha OBC na utalii wa picha (Thompson Safari Limited). Hivyo, katika mapendekezo au kusema nini kifanyike ni lazima mtu awe na muono mbadala.
Kwa upande wangu mimi napendekeza yafuatayo angalau yazingatiwe pale ambapo watunga sera, sheria, serikali na wadau wengine wenye maslahi katika ardhi au rasilimali zingine zinazopatikana Loliondo wawe na uwelewa na kuyatekeleza ili kutatua migogoro.
v Ushiriki wa wananchi; katika kulitatua tatizo la Loliondo au lingine lenye mtazamo sawa na huo ni lazima serikali na wadau wengine wawashirikishe wananchi katika kupanga matumizi ya rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao na sio kuwaona wananchi kama mzigo na wasio na uwelewa wa mambo kwani kutokuwajali wananchi (wazalishaji wadowadogo) ndiyo hupelekea serikali kushindwa kutekeleza mipango yake.
v Uwezeshwaji; wananchi wawezeshwe katika sehemu mbalimbali kama vile kiuchumi, kielimu, kisaikolojia, na kijamii pale ambapo kuna mradi au hata pasipo na mradi.
v Mbinu za jadi au kimila zinazotumika katika kutatua migogoro zitiliwe mkazo na zishirikishwe na za kiserikali ili kufikia muafaka kamili na kuachana na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali kuona kuwa mbinu za kimila zimepitwa na wakati.
v MMBA isifanywe kwa shinikizo na kwa muda mfupi kwa lengo la siasa za muda au kwa manufaa ya Wawekezaji bali liwe swala la muendelezo ambao ni huru na linajitegemea ili kuruhusu mawazo ya wenyeji kuwekwa katika utekelezaji.(LUP should be flexible).
v Pili isiwe pia kwasababu ya shinikizo la baadhi ya Wawekezaji kama OBC wenye kitalu pale Loliondo au Kampuni ya Utalii wa Picha ya Thompson Safari. Kwani Wawekezaji hao kwa kujua kuwa kuna uwelewa mdogo wa sheria miongoni mwa jamii zinazoishii katika eneo la Loliondo.
Hitimisho
Kwa ujumla ardhi ya Loliondo kama ardhi zingine chini ya utumiaji wa wafugaji na ambazo zimekuwa zikibadilishwa milki aidha na Rais kwa mamlaka aliyonayokisheria au mawaziri kwa mamlaka walizopewa na sheria hizohizo zisizorafiki na wafugaji inaweza kwenda mchana kweupe kwa shinikizo la Wawekezaji wenye maslahi pale na pia kwasababu ya viongozi wetu wa kiserikali au wa kisiasa wenye maslahi pia pale. Lakini zaidi ya yote zoezi linaloendelea lisilowashirikisha wananchi linaweza kulainisha ukwapuwaji wa ardhi hiyo na mwishoe kwa miaka kadhaa zijazo wananchi wa Tarafa yote ya Loliondo watahamishwa kwasababu si wakazi wa eneo hilo kama ilivyo tokea kwingineko Tanzania au hata hapo Loliondo mwaka 2009.
[1]
[2]
[3]
[4] Gazeti la Nipashe la Tarehe 25/02/2010